Kujiunga

Safari ya Malezi ya Kimonaki

"Ursberg," kama inavyo fahamika, ni jina la nyumba ya malezi ya abasia ya Ndanda. Mwanzoni mahali hapa palitumika kama shule ya kilimo chini ya uongozi wa marehemu Padre Ursus. Si ajabu basi nyumba iliyojengwa juu ya mlima huo mdogo inaitwa Ursberg. Ndugu Johannes Mango, mzaliwa wa kwanza wa Abasia kati ya ndugu Watanzania ni tunda la kundi la kwanza ambao waliingia mwaka1987. Walezi wa awali katika kundi la kwanza walikuwa Padre Hildebert Walter (1919-2006) na Padre Dionys Lindenmeier ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Abate wa Jumuiya.

Sifa za Wakandikati

Tunapokea waombaji kama wakandikati wetu baada ya kumaliza Kidato cha Nne. Wale wanao jisikia kuitwa kwa wito wa kipadre waweza kuendelea na Kidato cha Tano na Sita baada ya kuwa wamefaulu vizuri kidato cha nne. Wale ambao wanasikia wito wa kuwa mabradha wanapatiwa nafasi ya kujifunza ufundi stadi unaowaelekea. Hii ni pamoja na useremala. Fundi umeme, fundi ujenzi, ualimu, fundi bomba, uchapishaji wa vitabu, ufugaji, n.k.

 

Upostulanti

Tunapokea wakandikati kuwa wapostulanti baada ya masomo yao ya Kidato cha Sita au baada ya kupata daraja la pili katika ufundi stadi. Masharti: Lazima wawe wamefaulu mitihani yao ya taifa katika kidato cha nne, kidato cha sita au shule ya ufundi. Muda: Muda wa kuwa mpostulanti ni mwaka mmoja. Katika kipindi hiki wapostulanti wanakuwa wanapata vipindi vya darasani na kufanya kazi za mikono. Masomo yanatilia mkazo sala, mafundisho ya Kikristo, Biblia, liturjia na historia ya shirika letu. Mwanzoni mwa Mei hadi mwanzo wa Agosti, wapostulanti hufanya kazi za mikono katika karakana au idara zetu za kazi. Utaratibu huu umekuwa ukifanyika vizuri hadi sasa.

 

Unovisi

Muda wa unovisi ni miaka miwili. Katika mwaka wa kwanza wanovisi hukaa katika nyumba yetu ya malezi, na katika mwaka wa pili wanakaa monasterini na watawa wengine ili kujifunza na kujua maisha ya jumuiya. Muda huo wanovisi wanaendelea pia na vipindi vya darasani na pia kazi za mikono mpaka mwisho wa mwaka. Kwa mwezi mmoja hufanya kazi za mikono katika karakana zetu. Muda wote huu wanovisi wanayo fursa ya kujifunza juu ya Kanuni ya Mtakatifu Benedikto mwanzilishi wa shirika, Biblia, historia ya maisha ya kitawa, teolojia ya misioni, muziki, katiba ya shirika letu na maisha ya jumuiya. Pia wanapewa nafasi ya kujifunza mambo ya pekee kuhusu saikolojia, masuala kijinsia n.k.

 
 

Nadhiri za Muda & Malezi Endelevu

Kipindi cha unvovisi huhitimishwa kwa kufunga nadhiri za kwanza (nadhiri za muda) kwa kipindi cha miaka fulani. Kisha kupiga hatua hii muhimua katika safari ya kitawa, wale ambao wanasomea upadre wanaanza masomo seminari kuu. Wale wasiosomea upadre hujiunga na ndugu wengine katika karakana zetu kadiri ya ujuzi wao. Vipindi vya darasani huendelea kwa mabruda wote wenye nadhiri za muda kila jumatano kwa muda wa masaa mawili. Wana muda wa kutafakari (lectio divina) kila siku jioni kwa nusu saa. Ndugu hupata fursa ya kushiriki katika semina mbalimbali ili wasijepitwa na wakati. Kozi hizi zaweza kuwa mafunzo zaidi ya kiufundi, maisha ya kiroho, maarifa ya kiutawala, nk.

 

Vijana wanaotaka kujiunga wawasiliane na:

          Mkurugenzi wa Miito,

          Abasia ya Ndanda, SLP 25;

          Ndanda via Mtwara.

Wanaotoka maeneo ya Kaskazini ya Tanzania:

          Mkurugenzi wa Miito,

          SLP 40 Soni

          Lushoto Tanzania.

<<Mwanzo