Historia

 

HISTORIA YA ABASIA KWA UFUPI

BAADA YA WABENEDIKTINI wa kwanza kufika Tanganyika mwaka 1887, makao ya Papa huko Roma yaliunda eneo la kichungaji la kitume lililopewa jina “Zanzibar Kusini.” Historia ya abasia ya Ndanda, kwa hiyo, ina uhusiano wa karibu sana na eneo hilo la kitume. Wamisionari hao walijenga monasteri yao ya kwanza huko Pugu, Dar es Salaam, lakini kutokana na uasi wa Bushiri aliyekuwa anapingana na ukoloni wa Kijerumani, monasteri hiyo ilichomwa moto na hata baadhi ya watawa kupoteza maisha yao. Baada ya kuharibiwa kwa huko Pugu na hatima yake, mnamo mwaka 1894 Makao ya Papa yalimteua Pd. Maurus Hartmann kuwa Msimamizi wa Kitume wa “Zanzibar Kusini.” Eneo lake la kichungaji lilikuwa kama kilometa za mraba 400,000 hivi. 

Kushoto: Mwanzilishi na Mkuu wa Kwanza wa Shirika Pd. Andreas Amrhein. Kulia: Abate Placidus Mtunguja; 2015 - 

 

Wamisionari waliondoka Dar es Salaam na kuanza kazi za kitume maeneo ya Lukuledi na Nyangao – maeneo yapatikanayo siku hizi katika mkoa wa Lindi. Kati ya mwaka 1905 – 1907, wananchi wengi katika maeneo ya kusini mwa Tanganyika waliamua kupiga vita utawala wa kikoloni wa wakati huo. Vita hivyo vijulikanavyo kama Maji-Maji viliishia kuharibu vituo vingi vya misioni. Ni jambo la kushangaza kwamba, ingawa vita hivyo vilikuwa vinapamba moto bado, Askofu Thomas Spreiter alidiriki kuanzisha kituo kipya cha kimisionari Ndanda. Ilikuwa tarehe 15  Agoti 1906. Kuanzia wakati huo, Ndanda ilikuwa kituo muhimu zaidi cha kimisionari katika eneo lote la kusini mashariki mwa Tanganyika. Wakati wa vita vya kwanza vya Dunia, wamisionari wote walikuwa raia wa Ujerumani pamoja na Askofu Spreiter walifukuzwa kutoka nchini.

Kushoto: Joachim Ammanm, Abate Askofu I; 1932-1949. Kulia: Dionys Lindenmaier, Abate IV, 2001 - 2015

  

Huu ulikuwa ni wakati mgumu, lakini hata hivyo Ndanda ilizidi kuendelea na mnamo mwaka 1927, Ndanda pamoja na kituo kingine cha misioni cha Peramiho zilinyanyuliwa na kupewa hadhi ya kuwa abatia nullius (abasia ambaye mkubwa wake ana mamlaka kama ya askofu wa jimbo) iliyoitwa Lindi. Kiongozi wake alikuwa Abate Gallus Steiger. Mwaka 1931 eneo hili kubwa liligawanywa katika Abasia mbili huru nullius, Ndanda na Peramiho. Abate Gallus alibaki Peramiho na Joachim Ammann OSB akawa Abate wa kwanza wa Ndanda. Miaka miwili iliyofuata, Abate Gallus na Abate Joachim waliteuliwa kuwa maaskofu. Kutokana na uhakika wakupata wamisionari wapya, Ndanda iliweza kufungua vituo vingi vipya vya misioni na hivyo Kanisa liliweza  kuimarika na kukua.

Kushoto: Victor Haelg, Abate-Askofu II; 1949-1975. Kulia: Abate Siegfried Hertelein, abate wa II, 1976-2001

 

 

Mwaka 1938 kanisa jipya la Ndanda lilitabarukiwa. Hii iliashiria kuwa Ndanda ilikuwa inaendealea kuimarika. Vita vya pili vya dunia (1939-1945) vilikuwa ni tishio la kuharibu kila kitu tena. Wamisionari wengi Wakijerumani waliondoka, shule nyingi na vituo vilifungwa na Abate Joachim mwenyewe alikuwa mgonjwa. Miaka miwili baada ya vita (1947) alijuzulu wadhifa wake. Padri Viktor Haelg aliyekuwa msaidizi wake alichukua madaraka kama Abate-Askofu mwaka 1949. Chini ya uongozi wake kazi ya kimisionari iliendelea kwa mafanikio makubwa katika eneo lote la Umwera, Umakonde na hata maeneo ya pwani ambako kwa kawaida yalikuwa na ndugu Waislamu. Kwenye miaka 1960 Ndanda ilikuwa na takribani parokia 40, vigango 220, shule za msingi 200, hospitali 3, shule za kati 6 (mddle schools) na shule mashuhuri ya  sekondari ya Abasia Ndanda.

Kushoto. Br. Klemens, mmoja wa Wamisionari wa Kwanza: Kulia: Chifu Hatia na Mtawa wa Ndanda. 

 
 

Haya yote yalikuwa chini ya uangalizi wa Wamisionari kama 120, mapadri 10 wa jimbo, masista Wabenediktini wa Tutzing 50, Masista Wabenediktini wa Kitanzania wa jimbo 65 na Makatekista 250. Mwezi Desemba 1972 Abasia nullius ya Ndanda ilinyanyuliwa katika hadhi ya Jimbo. Katika kipindi hiki Askofu Victor Haelg aliweza kukabidhi uongozi wa kichungaji katika mipaka yake kwa Askofu mzalendo Maurus Libaba. Askofu Victor aliendelea kuwa Abate wa Ndanda kama Monasteri inayojitegemea ndani ya jimbo jipya la Mtwara. Katika wakati huo eneokubwa la Ndanda liligawanywa katika majimbo matatu: Mtwara, Lindi na Tunduru-Masasi ambayo kwa sasa linakadiriwa kuwa na Wakatoliki 260,000. Hawa wanahudumiwa na takribani Mapadri 120 wa Majimbo wakishirikiana na Masista Wazalendo kama 280.

 Kushoto: Mmojawapo wa Masista wa Tuzing walifanya kazi bega kwa bega na mapadre na mabradha wetu.
Kulia: Baadhi ya Watawa wa Ndanda katika picha ya pamoja mwaka 1928 - Ndanda.
 
 

Abate-Askofu Victor alifariki dunia Desemba 1975 na Februari mwaka 1976 Abate Siegfried Hertlein alichaguliwa kuwa mrithi wake. Hatua kwa hatua monasteri ilichukua mwelekeo mpya. Ni dhairi kuwa sasa imekuwa kituo cha Kimonaki na Nyumba Mama ya Wabenediktini Wamisionari. Tarehe 30 Novemba, 2000 Abate Siegfried alistaafu na jumuiya ilimchagua Abate Dionys Lindenmeier kama kiongozi wake mpya. Alipata Baraka 5 januari, 2001 na toka wakati huo amekuwa msimamizi mkuu wa shughuli za Abasia. Kadiri ya takwimu za mwaka 2011, jumuiya ilikuwa na jumla ya watawa 70.

Kushoto: Pd. Maurus Hartmann; Kulia: Afisa  wa Jeshi la Kijerumani Von Lettow wakati wa Vita vya I vya Dunia.

<<Mwanzo ** Matukio Muhimu >>

------------------------------