Wavovisi Wapya Wapokelewa

Wakati wa Dominika za kuombea miito huwa tunaaimba: "Bwana wa mavuno, peleka watenda kazi shambani mwako!" Mwenyezi alionekana kujibu sala hii moja kwa moja mwanzoni mwa Oktaba 2017 vijana sita walipoanza safari ya kujitayarisha kuishi maisha ya wakfu kwa kuingia novisiati katika utawa wetu. Kwa upande wa jumuiya yetu, tunaweza kusema kwamba tuna bahati au tunabarikiwa sana. Kwa miaka zaidi ya mitatu mfululizo, tumekuwa na neema ya kupokea vijana kati ya wanne hadi sita katika novisiati. Vijana hawa sita kama ishara ya maisha mapya walipewa majina mapya na Mkubwa wa Utawa. Majina haya ni ishara kwamba wapo katika njia mpya; njia tofauti. Tunawaombea neema na baraka katika safari hii nyeti waliyoanza. Ni sala na matumaini yetu kuwa vijana hawa watakuwa na sikio sikivu na mioyo mitulivu katika kumsikiliza Yesu aliye mwalimu na kiongozi wao. Tunasali kwamba Mwenyezi aliyewaita, akamilishe katika mioyo yao kile ambacho yeye mwenyewe amekianza.