Useremala

  KARAKANA YA USEREMALA  ni kati ya vitengo muhimu zaidi katika jumuiya yetu. Kitengo hiki kimekuwepo tangu awali kazi ya umisionari ilipoanza maeneo ya Ndanda. Kutoka katika karakana hii samani mbalimbali za nyumba na makanisa zimekuwa zinatengenezwa kwa umahiri mkubwa. Mafundi mahiri wa karakana hii wamefanya kazi kubwa za kuezeka nyumba, hospitali, mashule, vituo vya afya, vikanisa na makanisa makubwa katika sehemu mbalimbali.

 
  Tangu mwaka 1996 Bradha Benedict Mrema (juu kulia akikalia sofa aliyotengeneza) amekuwa akiongoza karakana hii akiwa na mafundi, wanafunzi na wasaidizi wegine zaidi ya 120. Kutokana na ubora katika uzalishaji kuongezeka; wigo wa wateja umeongezeka kujumuisha taasisi za serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), jimbo la Geita, Jimbo kuu la Dar es Salaaam (milango na viti vya kukalia kanisani kwa parokia za Sinza, Tabata, Mikocheni na Vikindu) na pia kwa ajili ya Usharika wa KKKT - Mabibo External Dar es Salaam.  
  Mbao ni mali ghafi mama katika karakana yoyote ya useremala. Karakana hii haitumii tu mbao. Ipo pia mstari wa mbele katika kupanda miti michanga na hivyo kutunza mazingira. Haishangazi, basi, kwamba Abasia ya Ndanda ilipata tuzo ya kitaifa huko Dodoma mwaka 2010 kwa kutambua mchango wetu katika kutunza mazingira. Kata mti, pandi MITI ndiyo sera yetu.  
         

<< Rudi Mwanzoni    **   SHOW ROOM   **   Wasiliana na Useremala >>